Islamic Calender

Powered by Blogger.

ELIMU YA HADITHI.


UCHAMBUZI YAKINIFU JUU YA ELIMU YA HADITHI.


Kabla ya kuanza kuzitaja hoja na dalili wanazozitegemea Ahli sunna
wal- Jamaa juu ya kuonekana Allah kwa macho huko akhera,
kwanza napenda kuzungumzia suala linalofungamana na elimu ya
istilahi ya upokezi wa riwaya za hadithi za bwana Mtume -swalla
llaahu alayhi wasallam- na suala hili litakuwa katika nukta
zifuatazo:

i) Kwanza, tufahamu kuwa mafundisho yote ya bwana Mtume -
swalla llaahu alayhi wasallam- ni wah’yi (ufunuo) utokao kwa
Allah, na Mtume -swalla llaahu alayhi wasallam- hazungumzi kwa
matashi wala matamanio ya nafsi yake.

ii) Pili, mafundisho yote ya Mtume wetu Muhammad -swalla llaahu
alayhi wasallam- yamehifadhiwa katika vitabu vya maulamaa wa Ahlu
Sunna wal-Jamaa kwa ufanisi mkubwa mno kiasi ambacho hakuna
jambo lolote linalohitajika kubainisha itikadi au hukumu ya mambo ya
dini ya kiislamu isipokuwa jambo hilo limedhibitiwa kwa ufanisi wa
hali ya juu.

iii) Tatu, katika kuhakikisha kuwa mafundisho hayo sahihi ya dini ya
kiislamu yanahifadhiwa na hayachanganyiki na upotofu wowote,
maulamaa wa Ahli Sunna wal Jamaa wameweka misingi madhubuti
juu ya usahihi wa mapokezi hayo ya riwaya za hadithi za bwana
Mtume -swalla llaahu alayhi wasallam- na ukweli wa wapokezi hao
kama tulivyofundishwa na Qur’an tukufu pale aliposema Allah:
ياأيها الذين آمنوا إن جاءآم فاسق بنبإ فتبينوا
“Enyi mlioamini ! akikujilieni mwovu (fasiki) na habari yoyote basi ichunguzeni”
al Hujraat (49) aya 6.
22
Kwa mujibu wa aya hii ni kwamba, si kila asemaye; amesema
Mtume -swalla llaahu alayhi wasallam- atakuwa msemaji huyo ni
mkweli, na atakayo yanukuu yatakuwa ni kweli maneno ya Mtume,
bali ni lazima uchunguzi wa kina ufanyike ili kujua usahihi wa habari
hiyo aliyoileta na udhaifu wake.
Kwa sababu hiyo, maulamaa wa hadithi baada ya kufanya utafiti wa
kina pamoja na kutumia uzoefu wao wa muda mrefu, wakaweka
misingi madhubuti inayowahusu wapokezi wa hadithi.
Pia wakaweka kanuni maalumu kwa ajili ya udhibiti wa njia sahihi
za kukubaliwa hadithi na kurudishwa.
Na pia yakatumika maneno ya kiistalahi ambayo yanaleta maana
maalumu na hayo yamejaa kwa wingi katika vitabu vyao.
Kwa mantiki hiyo, yeyote anayetaka kuzungumzia masuala
yanayofungamana na elimu ya hadithi; usahihi wake na udhaifu
wake, hana budi kuzijua kanuni hizo na maneno hayo ya kiistilahi.
Na kama hatafanya hivyo, basi lililobora kwake ni kunyamaza kuliko
kusema, kwa sababu hatima yake ni kupotosha watu kwa
kuzisahihisha hadithi zisizo sahihi au kuzidhoofisha hadithi zilizo sahihi
na yote mawili ni balaa, hasa ukizingatia kwamba maneno ya Mtume
Muhammad -swalla llaahu alayhi wasallam- ni sheria.
MASHAR’TI

YA USAHIHI WA HADITHI

العدالة ( 1 Uadilifu, ni lazima kila mpokezi wa hadithi za Mtume -
swalla llaahu alayhi wasallam- awe ni mtu mwenye akili
timamu,mwenye uwezo wa kupambanua mambo hata kama ni mtoto
mdogo, awe mkweli, mcha mungu na wala asiwe mwongo, zenye
kuvunja heshima.
23

تمام الضبط ( 2 Hifdhi nzuri wala asiwe mwenye kufanya maasia kwa
dhahiri wala asiwe na tabia mbaya
, mpokezi awe na uwezo wa kudhibiti maneno aliyo yapokea, bila
ya kubadilisha chochote katika maana yake,au kukosea sana,au
kubabaika kulikopetuka mipaka wakati wa kusimulia mapokezi hayo.

اتصال السند ( 3 Kuungana kwa sanadi (msururu wa wapokezi) kwa
kuwa kila mpokezi awe amepokea kutoka kwa aliye juu yake mpaka
mwisho wake (kwa huyo ambaye habari hiyo imenasibishwa kwake,
ima bwana -Mtume swalla llaahu alayhi wasallam-, au swahaba,
n.k.

عدم الشذوذ ( 4 Isiwe habari aliyoileta mpokezi huyo ni “SHAADHUN”
(ni yenye kupingana na habari ya mpokezi mwingine aliye madhubuti
au wengi zaidi kuliko yeye).

عدم العلة الخفية القادحة ( 5 Wala isiwe na ila (kasoro iliyojificha) kama
vile Idh’tiraabu (mgongano baina ya wapokezi n.k) au kuwa ni
habari Maq’luub (yenye kugeuzwa)
Katika masharti haya tuliyoyataja, yako ambayo likikosekana moja tu
basi hadithi haitakubaliwa,kama vile:
1-Kuwa mpokezi si muadilifu,kwa kuwa ni mwongo au asherati n.k.
2-Kupatikana kasoro kama vile mgongano katika sanadi (njia) au
mgongano wa maneno katika habari hiyo, kisha ikawa imeshindikana
kuziunganisha au kuipa nguvu njia moja juu ya nyingine.
Tanbihi:
Habari inaweza kuwa na njia nyingi, na katika njia hizo wakawepo
wapokezi wasio madhubuti kwa kuwa wanakosea kiasi, au silsila
(mtiririko) wa wapokezi haukuungana, kutokana na wingi wa njia
hizo habari hiyo itapata uzito na kuhesabiwa kuwa ni sahihi, na kwa
lugha ya kitaalamu huwa wanaiita “HASANUN-LIGHAIRIHI”.
24
Amesema Imamu An-Nawawiy:
"بل ما آان ضعفه لضعف حفظ راويه الصدوق الأمين من وجه آخر وصار حسناً وآذا إذا آان ضعفها
لإرسال زال بمجيئه من وجه آخر...".
“Bali ile hadithi ambayo imekuwa ni dhaifu kwa sababu ya udhaifu
wa mpokezi wake ambaye ni mkweli mwaminifu utaondoka (udhaifu
huo) kwa kuja kwake kupitia njia nyingine na itakuwa ni HASAN
(sahihi)
Na vile vile ukiwa udhaifu wake ni kwa sababu ya Ir’saal
(atakaposema Taabi’I amesema Mtume -swalla llaahu alayhi
wasallam-) pia udhaifu huo utaondoka kwa kuja (kupokewa) kwa
njia nyingine…”.
Hivyo basi, inawezekana ukaifuatilia hadithi kisha ukazikuta takriban
njia zake zote zina udhaifu, hapo hutakiwi kuwa na pupa na kuanza
kuihukumu hadithi yote kuwa ni dhaifu, bali unatakiwa kuihukumu
sanad husika tu, na useme kwamba sanad ya hadithi hii ni dhaifu.
Kwa sababu udhaifu wa sanad moja tu, si ushahidi wa udhaifu wa
hadithi yote yenye njia nyingi.
Na kama ukitaka kuihukumu hadithi yote kwa njia zake zote
unatakiwa ufanye kazi ya kuzikusanya sanad (njia) zote kisha ndiyo
uichambue sanad moja baada ya nyingine kwa kufuata kanuni na
taratibu za elimu ya hadithi (mustalahul-hadithi).
Na kama itakubainikia kuwa njia zote zina udhaifu, basi pia
unatakiwa kuangalia sababu za udhaifu wake.
Je udhaifu wake ni mwepesi au mzito?
Kama ni mwepesi basi hadithi hiyo kwa kuzijumuisha njia zote hizo
itakuwa ni “Hasanun-Lighayrihi” (sahihi) na itafaa kuifanya kuwa ni
hoja ya kisheria, na wala haitohesabiwa kuwa ni dhaifu.
Hili ni jambo muhimu sana katika elimu ya hadithi kulifahamu na
kulizingatia, lakini ndugu Juma kwa makusudi hakuuzingatia utaratibu
huu kwenye kitabu chake “Hoja zenye Nguvu” kwa sababu
anazozijua mwenyewe, kwani yeye ndiye aliyesema hivi:
25
“kitaalamu ikiwa hadithi imepokewa na wapokezi wengine kabisa,
lakini hadithi ni ile ile, basi huambiwa kuwa hadithi hiyo ina
shahidi.”
Mwisho wa kunukuu.
Tazama “Hoja zenye Nguvu” ukurasa 70.
Lakini huko mbele -Inshaallah- utazigumdua sababu zilizomfanya
ndugu Juma aupuuze utaratibu huu.
Source: hoja zenye nguvu katika kuthibitisha kuonekana allah(S.W) kwa macho huko akhera_Ukurasa 20-25)

Nguzo tano za uislam

Nguzo tano za uislam
1) Shahada ya Imani
Ushahidi wa Imani ni kusema kwa kusadikisha, La ilaaha illAllaah, Muhammadur Rasulullah.” Maana ya matamshi haya ni, “Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu (Allaah), na kwamba Muhammad ni Mjumbe (Mtume) wa Mwenyezi Mungu.” Sehemu ya kwanza, “Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki, isipokuwa Mwenyezi Mungu,” inamaanisha kwamba hapana mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu peke Yake, na kwamba Yeye hana mshirika wala mwana. Ushahidi huu wa Imani unaitwa Shahada, ambayo ni kanuni nyepesi ambayo inapaswa itamkwe pamoja na kusadiki ili mtu aweze kuingia katika Uislamu, kama ilivyoelezwa hapo juu. Ushahidi wa Imani ndio nguzo muhimu zaidi katika Uislamu.
2) Swalah
Waislamu huswali Swalah tano kila siku. Kila Swalah huchukuwa muda mfupi wa dakika chache tu. Swalah katika Uislamu ni mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mja na Mwenyezi Mungu. Hakuna kishenga baina ya Mwenyezi Mungu na mfanyaji ibada.
Ndani ya Swalah, mtu hujisikia ndani mwake furaha, amani na faraja, na kwamba Allaah yu radhi naye. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Bilaal adhini, ili tufarijike nayo.))[109] Bilaal alikuwa mmojawapo wa Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na alikuwa mwadhini.
Swalah hufanyika wakati wa Alfajiri, Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na ‘Ishaa. Muislam anaweza kuswali karibu mahali popote, kama vile mashambani, ofisini, viwandani au vyuoni.
Tafadhali, tembelea kwa ajili ya maelezo zaidi juu ya Swala katika Uislamu
3) Kutoa Zakaah (Kuwakunjulia Wenye Dhiki):
Kila kitu ni cha Mwenyezi Mungu, na hata mali zinazohifadhiwa na wanaadamu kama dhamana. Maana khalisi ya neno Zakaah ni zote mbili ‘kutwaharisha’ na ‘kukua.’ Maana ya kutoa Zakaah ni kutoa asilimia iliyotajwa bayana kutokana na mali fulani kwa kuwapatia makundi fulani ya watu wenye dhiki. Asilimia inayopaswa kulipwa kutokana na dhahabu, fedha na pesa taslimu zenye kufikia kiasi kinacholingana na gramu 85 za dhahabu na kubaki katika miliki ya mtu kwa mwaka mmoja wa Kiislamu ni asilimia mbili unusu. Tunavyovimiliki hutakasika kwa kutenga pembeni sehemu ndogo tu kwa ajili ya wenyedhiki, na kama vile kupogoa matawi ya mimea, huku kupunguza salio na kunatia moyo wa ukuaji mpya.
Mtu anaweza kutoa zaidi kadiri atakavyo kama Sadaka.
4) Kufunga katika Mwezi wa Ramadhaan Kila mwaka katika mwezi wa Ramadhaan,Waislamu hufunga tangu Alfajiri hadi kuchwa kwa jua, kwa kujizuia kula, kunywa na tendo la ndoa.
Ingawa Swawm ni yenye faida za kiafya, huchukuliwa kimsingi kuwa ni namna ya kuisafisha nafsi kiroho. Kwa mmojawapo kujizuia dhidi ya starehe za kidunia, japo kwa muda mfupi, mfungaji hupata huruma ya kweli kwa wanaopatwa na njaa, kadhalika na kuongezeka kwa maisha yake ya kiroho.
5) Kuhiji Makkah:
Hija ya kila mwaka Makkah ni faradhi ya kufanywa mara moja tu maishani kwa wenye uwezo wa kimwili na mali katika kuitekeleza. Kadiri ya watu milioni mbili huenda Makkah kila mwaka kutoka kila sehemu duniani. Ingawa mara zote Makkah huwa imesheheni wageni, Hija ya mwaka hufanywa katika mwezi wa kumi na mbili katika kalenda ya kiislamu. Mahaji wa kiume huvaa nguo maalumu na rahisi ambayo huondosha mbali tofauti za kimatabaka na tamaduni kiasi kwamba wote huwa sawa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Source:Al-Hidaya

HISTORIA YA MAWLID

HISTORIA YA MAWLID
Yeyote mwenye kutazama maisha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na historia ya Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum), Taabi‘iyna na waliowafuata kwa wema mpaka kufikia zaidi ya mwaka wa 350 Hijri hatumuoni hata mwanachuoni mmoja wala mahakimu (viongozi) na wala watu wa kawaida waliokuwa wakifanya Mawlid au wakaamrisha au wakahimiza au wakazungumza juu yake. Amesema al-Haafidh as-Sakhawiy: “Shughuli za kufanya Mawlid matukufu hayakupokelewa na watangu wema (Salafus Swaalih) wa karne tatu bora za mwanzo. Kwa hakika jambo hili lilizuliwa baada yake” (Imenukuliwa kutoka kwa Subulul Hudaa war Rashaad cha As-Salihiy, Mj. 1, uk. 439).
Suala la sisi kujiuliza ni kuwa;
Je, haya Mawlid yalianza lini?
Jawabu ya suala hili kwa mwanachuoni wa Ki-Sunnah, Al-Imaam al-Maqriiziyni:
“Katika kipindi cha uongozi wa Faatwimiyyuun (hawa walikuwa ni Rawaafidh (Mashia) katika kipote cha Ismailiyyah [Makoja] katika nchi ya Misri) walikuwa wanachukuwa hii ni misimu ya sherehe ambapo walikuwa wakiwakunjulia hali za raia zao na kuwakithirishia neema. Na walikuwa hawa watawala wa Faatwimiyyuun katika mwaka mzima wana misimu ya sherehe na Idi zao nazo ni kama zifuatazo: Msimu wa kichwa cha mwaka, Msimu wa mwanzo wa mwaka, Sherehe za ‘Aashuraa, na Mawlid ya Nabii (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Mawlid ya ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu), na Mawlid ya Hasan na Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhuma), na Mawlid ya Faatwimah az-Zahraa (Radhiya Allaahu ‘anha), na Mawlid ya kiongozi wao aliye hai kwa wakati ule, usiku wa kwanza wa Rajab, na usiku wa kati ya Rajab, na Mawlid ya usiku wa Ramadhaan na mwisho wa Ramadhaan na Msimu wa 'Iydul Fitwr na Msimu wa 'Iydul Adh-ha na Idi ya Ghaadir, Msimu wa ufunguzi wa Ghuba na Siku ya Nairuuz na Siku ya Ghatas na Siku ya Mazazi, na Siku ya Vipandio, Kis-wa (nguo) ya Msimu wa Kusi na Kaskazi, Alhamisi ya Adasi na Siku ya Ubatizo” (Al-Khutwat, Mj. 1, uk. 490 na baada yake). na amesema tena katika kitabu chengine: “Na katika mwezi wa Rabi’ul Awwal walijilazimisha watu kuwasha kandili usiku katika njia zote na vichochoro vyake huko Misri”.
Na amesema tena al-Maqriiziy katika maudhui nyengine: “Shughuli za Mawlid ya Mtume mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilikuwa zikifanyika rasmi kama desturi yake katika mwezi wa Rabi’ul Awwal”. Kila mmoja anatakiwa azingatie jinsi gani Mawlid yalivyoanzishwa pamoja na uzushi mkubwa mfano: Uzushi wa kukataa na kuchupa mipaka juu ya familia ya Mtume kwa kusimamisha mawlid ya ‘Aliy, Faatwimah, Hasan na Husayn.
Uzushi wa kusherehekea Idi ya Nayruuz, na Idi ya Ghatas na kuzaliwa kwa Masihi nazo ni Idi za Wakristo. Amesema Ibn Turkumani kuhusu hizi Idi za Wakristo: “Na miongoni mwa uzushi inayoleta hizaya ni wanaofanya Waislamu katika siku ya Nayruuz ya Kikristo na misimu yao mengine na siku kuu (Idi) kwa kupeana chakula kwa wingi. Na sadaka ya chakula isiyokubalika itarudi kwa mwenye kutoa kwa haraka au baadae. Na kwa uchache wa tawfiki na kufaulu ni yale wanayofanya Waislamu waovu kwa inayotambuliwa kama siku ya mazazi (yaani kuzaliwa kwa Yesu)” (Al-Lam‘i Fil Hawaadith wal Bid’ah, Mj. 1, uk. 293 – 316). Na imenukuliwa kutoka kwa wanavyuoni wa Hanafiyyah kwamba yeyote ambaye atafanya mambo yaliyotangulia atakuwa kafiri mfano wao (hao Wakristo). Na wakataja idadi za Idi kadhaa za Wakristo ambao Waislamu walio wajinga wanashiriki, na jinsi zilivyo uharamu wake katika Kitabu na Sunnah na yale misingi ya kisheria yaliyo kamili.
Watu wa kwanza kuzua kile kinachoitwa Mawlid ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Bani ‘Ubayd ambao walikuwa wakijulikana kama Faatwimiyyuun. Haya yametajwa na wanazuoni wengi mfano Mufti wa Misri wa zamani, Shaykh Muhammad Bakhiit al-Mutii‘y katika kitabu chake Ahsanul Kalaam Fi maa Yata‘alaq Bis Sunnah wal Bid‘ah Minal Ahkaam; Shaykh ‘Ali Mahfuudh katika kitabu chake Al-Ibda‘ Fii Madh-har al-Ibtidaa‘; Shaykh Isma‘iyl al-Answaariy katika kitabu chake Al-Qawlul Fasl Fiy Hukmil Ihtifaal Bi Mawlid Khayrir Rasuul.
“Wa mwanzo walioyazua Mawlid huko Cairo ni watawala wa Kifaatwimiyyah (Mashia) katika karne ya nne. Walizua Mawlid aina sita: Mawlid ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Mawlid ya Imam ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu), Mawlid ya Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha), Mawlid ya Hasan (Radhiya Allaahu ‘anhu), Mawlid ya Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhu) na Mawlid ya Khalifa aliyekuwepo” (‘Ali Mahfuudh katika kitabu chake al-Ibda‘ Fii Madh-har al-Ibtidaa‘, uk. 251).
Je, wanazuoni wamesema nini kuhusu hii Dola ya Faatwimiyyuun ‘Ubaydiyyah ambayo imeanzisha jambo hili (Mawlid ya Mtume)? Amesema Imaam Shaamah, mwana-historia na Muhaddith (aliyeboboea katika mas-ala ya Hadithi za Mtume [Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam]), mwandishi wa kitabu ar-Rawdhatayn Fiy Akhbaar Dawlatayn, uk. 200 – 202 kuhusu Faatwimiyyuun ‘Ubaydiyyah: “Wao walijidhihirisha kwa watu kuwa wao ni masharifu (watukufu) kutoka kwa Faatwimah hivyo wakamiliki na kutawala ardhi na kuwatendesha nguvu waja. Na wametaja kipote cha wanazuoni wakubwa kuwa wao hawakustahiki hilo na nasaba yao si sahihi bali walikuwa wanajulikana zaidi kwa banu ‘Ubayd. Na baba wa ‘Ubayd alikuwa ni katika kizazi cha wakanaji Mungu na Mmajusi na inasemekana kuwa babake alikuwa Myahudi mfua vyuma kutoka Shaam. Jina la huyu ‘Ubayd lilikuwa ni Sa‘iyd, lakini alipofika Morocco alijiita ‘Ubaydullah na akajidai kuwa yeye ni katika ukoo wa ‘Alawi Faatwimiy na madai yake ya nasaba hiyo siyo sahihi. Yeye hakutajwa na yeyote miongoni mwa wajuzi wa nasaba za ‘Alawi, kipote kikubwa cha wanavyuoni wametaja kinyume cha hayo. Alijinasibisha na Bani Mahdiyyah wa Morocco, naye alikuwa Zindiyq muovu, adui wa Uislamu na alijidhihirisha Ushia wake. Alikuwa na hima ya kuiondoa mila ya Kiislamu pamoja na kuwaua mafaqihi wengi pamoja na wanavyuoni wa Hadiyth. Kusudio lake kubwa lilikuwa kuwaondosha kabisa ili dunia ibaki na wanyama pekee na hivyo kumakinika katika kuleta uharibifu katika itikadi zao na kuwapoteza lakini Allaah Anaitimiza nuru Yake japokuwa watachukia makafiri”. 
Kizazi chake kiliinukia katika hilo huku wakijitokeza wakati kukiwa na fursa na isipokuwa hivyo walikuwa wakijificha na kufanya vituko vyao kwa siri. Walinganizi wake walitumwa katika nchi yote huku wakiwapoteza wale wanaoweza miongoni mwa waja. Balaa hii ilibakia kwa Uislamu kuanzia mwanzo wa Dola yao mpaka mwisho wake yaani Dhul-Hijjah 299 hadi 567 Hijri.
Katika siku zao za utawala hawa Rawaafidh (Mashia) waliongezeka sana na hivyo wakawa wanahukumu watu kwa kuwawekea vikwazo na wakaweza kuharibu itikadi za mapote ya watu waliokuwa wakiishi katika majabali na mapango ya Shaam kama Nusayriyyah, Druze na Hashashiyyun (Assassins), wote wakiwa aina moja na wao wenyewe. Waliweza kuwatumia kwa sababu ya udhaifu wa akili zao na ujinga wao, hivyo kuwapatia fursa Wazungu (Crusaders â€“ watu wa msalaba) kuziteka ardhi za Shaam na Bara Arabu mpaka Allaah Alipowapatia Waislamu ushindi chini ya uongozi wa Swalaah ud Diyn Hasan al-Ayyubi ambaye aliweza kuzirudisha nchi hizo kwa Waislamu.
Makhalifa 14 walipita, ambao walikuwa wanajiita masharifu na nasaba yao ni kutokana na Majusi au Mayahudi mpaka likawa maarufu baina ya watu wa kawaida hivyo kuiita dola hiyo, Dola ya Faatwimah na Dola ya ‘Alawi na ilihali uhakika ni Dola ya Kimajusi au ya Kiyahudi wakanaji Mungu.
Na miongoni mwa uovu wao ni kuwa walikuwa wakiwaamrisha makhatibu kwa hilo (yaani wao ni Alawiyyah Faatwimiyyuun) na hayo yalikuwa yakisemwa juu ya minbar na wakiandika katika kuta za Misikiti na sehemu nyinginezo. Na alihutubu yeye mwenyewe mtumishi wao kwa jina Jawhar, aliyeteka nchi ya Misri na kujenga mji wa Cairo. Alisema ndani yake: “Ewe Mola mswalie mja wako na rafiki yako tunda la Unabii na dhuria wako mwenye kuongoza muongofu anayepelekesha mambo. Naye ni Abi Tamiym Imam Mu‘iz-ud-Diinil Llah, Amiri wa Waumini kama ulivyowaswalia baba zake walio tohara na waliomtangulia kwa kuchaguliwa, maimamu waongofu”. Amesema uongo adui wa Allaah, hakuna kheri kwake wala kwa watangu wake wote wala kwa dhuria wake waliobakia na kizazi cha Unabii tohara miongoni mwao.
Na yule mwenye lakabu ya Mahdi, laana ya Allaah iwe juu yake aliwachukuwa wajinga na kuwasalitisha kwao wale wenye fadhila.. Alikuwa akiwatuma kwenda kuwachinja mafakihi na wanavyuoni katika firasha zao. Na akawasaliti Waislamu kwa Warumi na alikuwa na ujeuri mwingi na kuchezea mali na kuwaua watu. Alikuwa na kipote cha walinganizi (ma-Du‘aat) wake waliokuwa wakifanya kazi ya kuwapoteza watu kwa uwezo wao wote.. Wao walikuwa wakiwaambia baadhi ya watu: “Huyo ni Mahdi mtoto wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na dalili (huja) ya Allaah kwa viumbe vyake”. Na kwa wengine: “Huyu ni Mtume wa Allaah na dalili ya Allaah”. Na kwa wengine: “Yeye ni Allaah, Muumbaji, Mwenye kuruzuku”. Hapana Mola muabudiwa wa haki ila Allaah tu, Naye Hana mshirika, Ametukuka na Hana upungufu wala kasoro aina yoyote kwa yale wanayoyasema madhalimu kwa kiburi kikuu. Alipoangamia alichukua hatamu za uongozi mtoto wake anayeitwa, Qa’im, naye alizidisha shari yake juu ya uovu wa babake maradufu. Akatoka na kuwatusi Manabii na alikuwa akinadi masokoni na sehemu nyenginezo: “Mlaanini ‘Aishah na mumewe. Mlaanini pango na vinavyounganishwa”.
Ewe Allaah! Mswalie Nabii Wako na Maswahaba zake na wakeze walio twahara na uwalaani hawa makafiri walioasi na kuvuka mipaka katika ukanaji wa Mwenyezi Mungu na Uwarehemu waliopambana nao na ikawa ndio sababu ya kuing’oa mizizi na utawala wao. Waislamu katika zama za utawala wao walipata dhiki na shida kubwa kwa ukatili, kiburi na ujeuri wao uliochupa mipaka.
Na juu ya Mawlid ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama tulivyoona asli yake na mwanzilishi wake ni kutokamana na Baatwiniyyuun (Faatwimiyyuun) waliokuwa na asli ya Kimajusi Kiyahudi waliohuisha mwito wa watu wa msalaba. Na hapa tunawaambia ya kwamba: Je, inajuzu na kusihi kuifanya chimbuko letu katika 'Ibaadah ni kutoka kwa watu hawa? Nasi tunarudia mara nyingine tena kuwa zile karne zilizo bora na kufadhilishwa ambazo waliishi watangu wetu wema hakukuwa na athari wala kufanywa mfano wa hizi 'Ibaadah. Hawakufanya wao wala wale waliokuwa na uadui nao na hata wale wajinga katika watu wa zama hizo na watu wa kawaida. Basi nasi hatujishughulishi katika yale waliyoyafanya na kujishughulisha nayo wao.
Naye Shaykh 'Abdulla Saleh Farsy (Allaah Amrehemu) katika kuelezea yalivyoanza Mawlid anasema:
"Walioanza Mawlid ni watu wenye Madhehebu za Kishia, hawa Shia Ismailiya walizitawala nchi za Kisuni tangu mwaka 297 A.H. (909) mpaka 567 A.H. (1171) (muda wa miaka 270).
Walipotoka katika nchi hizo waliacha hiyo ada yao ya kumsomea Mawlid Mtume na Maimamu zao. Basi Suni wakaendeleza Mawlid ya Mtume, wakayawacha yote mengine.
Mawlid ya Mwanzo Rasmi Kusomwa na Suni:
Mawlid ya mwanzo Rasmi yalisomwa na Suni ni Mawlid aliyokuwa akiyasoma Mfalme Mudhaffar Din- Mfalme wa kaskazi ya Iraq ambaye alikuwa shemeji wa mfalme mkubwa wa Kiislamu, Mfalme Salahud Din (Saladin - maarufu). Mawlid makubwa kabisa hayo. Yalikuwa yanahudhuriwa na watu wa pande zote zilizokuwa karibu na hapo, kwa shangwe kubwa kabisa lisilokuwa na mfano.
Mfalme huyo alizaliwa mwaka 549 A.H. (1154 wa kizungu); na akatawala hapo mwaka 586 A.H. (1190) na akafa 630 A.H. (1233) - miaka mia saba na khamsini na sita (756) kwa tarikhi ya kiislamu, na miaka mia saba na thalathini na tatu kwa tarikhi ya Kizungu. Basi ada ya kusoma Mawlid haikuanza miaka mingi sana. (Tafsiri ya Mawlid BARZANJI - KADHI SHEIKH ABDULLA SALEH FARSY, ZANZIBAR, Uk.(iv) )

Sababu za Kutosherehekee Maulidi-Sehemu ya Kwanza


 sehemu ya kwanza
Sababu 21 Za Kumfanya Muislam Asisherehekee Maulid
 Zifuatazo ni sababu na hoja ambazo Muislam mwenye kupenda kufuata haki na mwenye kutaka apate uongofu ili abakie katika njia iliyonyooka na ajiepushe na mambo ya baatil. Hoja ni za wazi kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Hoja za kupinga jambo hili ziko nyingi sana, lakini tulizozikusanya tunatumai kuwa zitamtosheleza Muislamu aikinaishe nafsi yake kuwa Maulidi ni jambo la uzushi katika dini kwa hiyo ni bora kutenda amali zile tulizopata mafundisho yake kutoka kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم, Maswahaba wake na Salafus Swaalih (Watangu wema) .
SABABU YA KWANZA: Kumpenda Mola Mtukufu Aliyetuumba:
Kwanza kabisa ni kwa sababu  ya kumpenda Mola Mtukufu Aliyetuumba Ambaye Anataka kuhakikisha kuwa mapenzi yetu Kwake ni kumfuata Mtume صلى الله عليه وآله وسلم. Naye tokea kuzaliwa kwake hadi kufa kwake hakufanyiwa wala hakusherehekea siku yake ya kuzaliwa. 
 Anasema Allaah سبحانه وتعالى :
 ((قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَاللّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ)) 
 ((Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Allaah basi nifuateni mimi, Allaah Atakupendeni na Atakufutieni madhambi yenu. Na Allaah ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu)) [Al-'Imraan: 31] 
 SABABU YA PILI: Kufuata amri yake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم    ya kushikamana na Sunnah Zake na Sunnah za Makhalifa wake:
 (( أُوصِيكُمْ بِتَقْوى اللَّه، وَالسَّمْعِ وَالطَّاعَةِ وإِنْ تَأَمَّر عَلَيْكُمْ عَبْدٌ حبشيٌ ، وَأَنَّهُ مَنْ يَعِشْ مِنْكُمْ فَسَيرى اخْتِلافاً كثِيرا . فَعَلَيْكُمْ بسُنَّتي وَسُنَّةِ الْخُلُفَاءِ الرَّاشِدِينَ الْمَهْدِيِّينَ ، عضُّوا عَلَيْهَا بالنَّواجِذِ ، وإِيَّاكُمْ ومُحْدثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٍ ضلالَةٌ ))  رواه أبو داود ، والترمذِي وقال حديث حسن صحيح
((Nakuusieni kumcha Allah, usikivu na twaa hata ikiwa kiongozi wenu (Au atakayekuamrishen) ni Mtumwa  wa Habash. Mtakaoishi miongoni mwenu mtaona ikhtilafu nyingi. Kwa hiyo shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waliongoka baada yangu.  Ziumeni kwa magego (zikamateni kwa nguvu wala msiziache). Na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu)) [Abu Daawuud, At-Trimidhiy kasema Hadiyth Hasan Swahiyh]   
Kwa hiyo inamtosheleza Muislamu hoja hii pekee ya kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم wala Maswahaba zake hawakusherehekea Maulidi, kumfanya naye asisherehekee.
Na hiyo ndio sababu kubwa ya Waislamu kukhitilafiana na kugawanyika makundi makundi. Amesema Imaam Maalik رحمه الله "'Hakuna kitakachotengeneza Ummah huu wa mwisho ila kwa kile kilichotengeneza Ummah wa mwanzo". Na maadam Salafus-Swaalih (watangu wema) hawakufanya bid'ah kama hii, sisi ni lazima tuwe na khofu kubwa ya kuifanya.

SABABU YA TATU:  Ametuamrisha Allaah سبحانه وتعالى tufuate aliyotuletea Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na tujiepushe na aliyotukataza:
    ((وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا))
 ((Na anachokupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho)) [Al-Hashr:7]
 SABABU YA NNE: Kufuata amri ya Kumtii Allaah سبحانه وتعالى na Mtume Wake صلى الله عليه وآله وسلم :
 Anasema Allaah سبحانه وتعالى katika Aayah nyingi kwenye Qur-aan:
 ((وَأَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ))
 ((Na mtiini Allaah na mtiini Mtume )) [At-Twaghaabun:12]
 Na kumtii Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ni kumtii Allaah سبحانه وتعالى
 ((مَّنْ يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللّهَ))
 ((Mwenye kumtii Mtume basi ndio amemtii Allaah)) [An-Nisaa:80]
 SABABU YA TANO: Kutokufuata amri ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ni kumkhalifu na kupata adhabu kali:
   ((فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيم))

((Basi nawatahadhari wanaokhalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu chungu)) [An-Nuur:63]
 SABABU YA SITA:  Kumpinga Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ni sababu ya kuingizwa toni:

 ((وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَى وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّى وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ وَسَاءتْ مَصِيرًا))
 ((Na anayempinga Mtume baada ya kumdhihirikia uongofu, na akafuata njia isiyo kuwa ya Waumini, tutamuelekeza alikoelekea, na tutamuingiza katika Jahannamu. Na hayo ni marejeo maovu)) [An-Nisaa 115]
 SABABU YA SABA: Kukhofu upotofu unaompeleka mtu motoni:
   Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Alikuwa akitanguliza khutba zake kwa kutoa maonyo hayo:
 (( إن خير الكلام كلام الله وخير الهدي هدي محمد صلى الله علي وسلم  وشر الأمور محدثاتها وكل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة وكل ضلالة في النار))  أخرجه مسلم في صحيحه 
 ((Maneno bora  ni kitabu cha Allah (Qur-aan) na Uongofu mbora kabisa ni uongofu wa Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم  na jambo la shari kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya (katika dini) ni bid'ah (uzushi)  na kila bid'ah ni motoni)) [Muslim katika Swahiyh yake]
 SABABU YA NANE:  Khofu ya kuwa miongoni mwa kundi litakaloingia motoni:
  Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipoonya katika Hadiyth ifuatayo kuwa makundi yote yanayojiita ni ya Kiislam na hali hayafuati mafunzo kama aliyokuja nayo yeye, yatakuwa motoni isipokuwa kundi moja. Maswahaba walishtuka na wakataka kujua ni kundi gani hilo moja, akawajibu kuwa ni kundi ambalo watu wake watakuwa wanafuata mwendo wake na wa Maswahaba zake.
 ((افترقت اليهود على إحدى وسبعين فرقة، وافترقت النصارى على اثنتين وسبعين فرقة، وستفترق هذه الأمة على ثلاث وسبعين فرقة كلها في النار إلا واحدة،)) فقال الصحابة: من هي يا رسول الله؟ قال: ((من كان على مثل ما أنا عليه وأصحابي)) الترمذي و الحاكم
 ((Waligawanyika Mayahudi katika makundi sabini na moja, na waligawanyika Manaswara katika makundi sabini na mbili, na utagawanyika Umma wangu katika makundi sabini na tatu, yote yataingia motoni ila moja!)) Maswahaba wakasema: 'Ni kundi lipi hilo Ee Mtume wa Allaah?  Akajibu: ((Ni lile ambalo litakuwa katika mwenendo wangu hii leo na Maswahaba zangu)) [Imepokewa na Maimaam At-Tirmidhiy na Al-Haakim]
 SABABU YA TISA: Kuitikia wasiya wa Allaah سبحانه وتعالى  ili kubakia katika njia iliyonyooka:
 Anasema Allaah سبحانه وتعالى :
  ((وَأَنَّ هَذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ذَلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ))
 ((Na kwa hakika hii ndiyo Njia Yangu Iliyonyooka. Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya Amekuusieni ili mpate kumcha Mungu)) [Al-An'aam: 153]
 inaendelea

 

Website Hit