Islamic Calender

Powered by Blogger.

YEPI YA KUIMARISHA UDUGU WETU WA KIISLAMU ?

Yepi Ya Kuimarisha Udugu Wetu Wa Kiislamu ?

Kwa mujibu wa tovuti moja ya Kiislamu, idadi ya Waislamu duniani inafikia bilioni 1.6. Hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 235 (235%) kwa kipindi cha miaka hamsini iliyopita.
Kwa idadi kubwa namna hii ya wafuasi, tungeweza kabisa kutimiza malengo yetu. Lakini jicho la utafiti katika jamii ya Waislamu hivi leo linaonesha picha tofauti kabisa-ni picha ya jeshi lililoshindwa kupambana na wengine-matokeo yake ardhi yetu, mali zetu na rasilimali nyinginezo zote ziko mikononi mwao.

Kwa kweli Umma wetu uko katika mazingira ya kutisha. Tumefika hapo kwa sababu sisi wenyewe tumeuacha Umma wetu ugawanyike na tumepuuzia umuhimu wa kukuza na kuimarisha mafungamano ya udugu wetu wa imani.

Kwa kupoteza mafungamano haya muhimu mno ya udugu wa Kiislamu ambayo, huko nyuma, ndiyo yaliyowaletea mafanikio Maswahaba, sasa tumekuwa umma mnyonge.

Ni pale tu tutakaporejesha mafungamano haya ndipo tutakapoweza kuondokana na unyonge na kurejesha uhuru na hadhi ambayo Umma wetu ulikuwa nayo huko nyuma.

      “Kwa hakika Waislamu wote ni ndugu...” (49:10).
Katika Aya hii, MwenyeziMungu anatuelezea kama Umma mmoja (ndugu). Mbali ya ukweli kuwa sote ni watoto wa baba mmoja (Adam) na mama mmoja (Hawwa),  pia tunapaswa kuwa ndugu wa imani, na huu ndio udugu hasa wa kweli.

Pale Waislamu walipofanya hijira kutoka Maka kwenda Madina, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuomba kila mwenyeji mmoja wa Madina (Ansari) ampatie makazi Muhajiri mmoja, na amlishe na kuvisha vile vile kama anavyokula na kuvaa yeye.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alielewa umuhimu wa kujenga udugu imara tangu mwanzo ili kujenga jamii bora na imara ya Kiislamu. Hatuwa yake hii ya hekima ikawezesha kuwepo kwa mapenzi na udugu wa dhati kati ya Ansari na Muhajirina na udugu huu ndio uliounganisha makabila mbalimbali ya Warabu kwa msingi mmoja wa Kalima “hakuna Mola isipokuwa Allah na Muhammad ni Mtume Wake”.

Kama kweli Waislamu wa leo tunataka kufanikiwa basi hatuna budi pia kupendana kwa ajili ya MwenyeziMungu. Ili kuimarisha udugu wetu, lazima tuanze na nafsi zetu.

Endapo tutaweza kuwa na khulka njema mbele ya Waislamu tunaokutana nao, hilo, InshaAllah ndilo litakaloanza kuleta athari ambayo, kidogo kidogo itauathiri Umma mzima. Ili kuleta mabadiliko, tunapaswa kutekeleza haya:

Mara zote tuwatendee ndugu zetu katika imani vile vile ambavyo nafsi zetu zingependa kutendewa. Na tuepuke kuwatendea vile ambavyo nafsi zetu zisingependa kutendewa.

Anas kasimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema,
“Hawi muumini mmoja wenu mpaka ampendelee nduguye kile inachopenda nafsi yake.” (Bukhari).

Ikiwa ni hatuwa ya kwanza twaweza kuanza kwa jambo ambalo twaweza kuliona dogo tu lakini ni jambo linalowezekana kwa kila mmoja wetu. Jambo hili ni la kujiombea dua sisi wenyewe na kuwaombea dua Waislamu wenzetu.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema,
“duwa ya Muislamu kumuombea nduguye Muislamu bila mwenyewe kujuwa ni duwa inayokubalika na atahudhurishwa Malaika. Kila akimuombea dua nduguye (Muislamu), Malaika huyo ataitikia, “Amiin”. (Muslim).

Undani wa jambo hili una umuhimu mkubwa katika kujenga udugu wa dhati. Duwa hiyo ambayo mtu anamuombea Muislamu mwenzie ni ya kheri kwa maana ya kumtakia mema.

Hapa tayari anakuwa amejenga hisia za kumjali na kumpendelea mema nduguye huyo. Hali hii ikishazoeleka nafsini, udugu wa kweli huanza kudhihiri katika matendo.

Kwamba yule yule aliyemtakia kheri katika dua, kimaumbile, atampendelea na mambo mengine mema anayoyapenda yeye. Atampendelea chakula anachokula yeye, atampendelea mavazi anayovaa yeye na kadhalika. Kwa ujumla na kwa kila hali Muislamu huyo atajitahidi kumridhisha nduguye.

Kwa kadri iwezekanavyo, ni muhimu kwa ndugu wa Kiislamu kusali Sala zao za faradhi kwa jamaa. Si tu jambo hili linaileta jamii pamoja, bali pia Allah huziunganisha nyoyo zetu tufanyapo Ibada pamoja.

Aidha ni jambo muhimu kutembeleana na kujuliana hali nyakati za mitihani ya ugonjwa au maradhi na katika shida nyinginezo. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameripotiwa kusema:

“Wale wamsaidiao Muislamu katika shida za dunia hii watakingwa na Allah wasipate shida za Akhera”. (Muslim).

Tunapaswa kuwa mfano bora wa ukarimu na huruma kwa kila mmoja wetu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) karipotiwa kusema: “Utawaona Waislamu wakipendana na kuhurumiana mithili ya kiwiliwili kimoja; iwapo kiungo chochote ni kigonjwa basi mwili wote huumwa na kukosa usingizi”. (Bukhari)

Tuwe waadilifu na waaminifu kwa kuchungiana heshima. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameripotiwa kusema,
“mmoja wenu akilinda heshima ya nduguye, MwenyeziMungu Atauweka Moto wa Jahanamu mbali na uso wake Akhera. (Muslim).

Ni jambo lenye faida kubwa katika udugu wa Kiislamu kukirimiana. Kila mmoja amfanyie takrima mwingine kwa kadri ya wasaa wake. Katika kukirimiana, sio mpaka kila mmoja wetu aende nyumbani kwa mwenziwe kwani wakati mwingine majukumu hututinga kiasi kwamba muda hautoshi. Ipo njia nyingine nzuri ya kufanyiana takrima.

Nayo ni “kuonjeshana mapishi ”. Hii ikiwa na maana ya kupelekeana vyakula hata kwa kiasi kidogo. Huyu anapika tambi na yule anakamua juisi. Kila mmoja anapeleka kwa mwingine kile alichoandaa.

Tusijali kiasi, hata glasi moja ya juisi inatosha na japo tambi katika kisahani kimoja cha chai zinatosha. Kwani kinachokusudiwa hapa sio kushibisha matumbo bali kulainisha nafsi zetu.
Hii ni kutokana na ukweli kuwa kila mmoja hakuridhika kula tambi zake au kunywa juisi yake bila kumshirikisha nduguye Muislamu. Hapa inatimia ile Hadith ya Mtume kuwa tupendeleane nafsi.

Isipokuwa tujihadhari kuwa Shetani anaweza kuzitekanyara takrima zetu na kuzigeuza kuwa “fahari”. Kwamba kila mmoja anataka ‘kumuonesha mwingine ‘jeuri’ yake ya mapishi au kutaka ajue nini kapika leo nyumbani kwake.

Matokeo ya hili ni kuwa mtu huionea aibu riziki yake aliyoruzukiwa. Siku akipiga ugali na mlenda, hapeleki kwa mwenziwe kwa hofu kuwa ‘atajidhalilisha” wakati falsafa ya kupeana ni tofauti kabisa. Kinacholengwa sio chakula bali kinacholengwa ni nafsi.

Kama mtu atatoa ugali na mlenda kwa mapenzi kuwa ‘na ndugu yake ashiriki kula hicho ambacho yeye anakula kwa siku hiyo, basi ugali huo huo na mlenda utatimiza lengo la Hadith ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa kila mmoja wetu ampendelee mwingine kile akipendacho’.

Hata kama yule anayepelekewa hakipendi chakula hicho na pengine akakimwagilia mbali jaani, lakini kwa kuwa kilichokusudiwa sio chakula, bado na yeye atahisi kitu fulani katika nafsi yake.

Atahisi kuwa nduguye Muislamu amempendelea kile alichonacho kwa siku hiyo. Na labda hiyo itakuwa fursa kwake ya kujuwa kuwa kumbe wakati yeye anakula wali na kuku, nduguye anakula chakula hicho.

Kwa kuwa ataguswa na jambo hili, naye atalazimishwa na hisia kupeleka kwa nduguye huyo huo wali na kuku anaokula. Hapa kinatimia kilichokusudiwa nacho ni kujenga hisia za kutendeana wema.

Jambo moja la kuangaliwa sana ni kwamba takrima ya vinono kila siku inaweza kukwama. Kutokana na hali duni za maisha katika familia zetu nyingi, si mara zote yatapatikana mapochopocho ya kupelekeana.

Isipoangaliwa, takrima inaweza kuwa ya upande mmoja tu wenye uwezo wa kupata mapochopocho. Lakini upande mwingine haujibu takrima kwa sababu ya kuona aibu kupeleka kisamvu kwa mwenziwe aliyemletea maini ya ng’ombe.
Ukarimu wa upande mmoja tu hauleti tija kubwa katika ujenzi wa udugu wa imani. Upande mmoja ukijiona mnyonge na hivyo kustahili kupewa tu bila wenyewe kuwapa wengine, hautatimiza Hadith ya kukirimiana.

Hivyo mtu asijipe haki ya kupewa tu kila siku. Kwamba akiletewa sahani ya tambi azile tu na kisha kuosha sahani na kuirudisha tupu kule ilikotoka. Sahani ya takrima lazima irejee na takrima. Mtu akipelekewa sahani ya magimbi naye atiye alichonacho katika sahani hiyo ili kujibu takrima aliyofanyiwa. Hata matunda mawili -matatu yanatosha.

Tukizichunga nafsi zetu na ria, basi jambo hili litasaidia mno kujenga mapenzi miongoni mwetu. Tunapopelekeana vyakula, tuhakikishe tunakificha machoni mwa watu. Sio mtu anapita na sahani ya chakula waziwazi na kufanya watu wote wajuwe kuwa anapeleka chakula kwa fulani!

Kumbukumbu bado ipo kuwa tabia ya kukirimiana kwa kupelekeana vyakula ilikuwepo huko nyuma katika jamii zetu hasahasa nyakati za Ramadhani.

Lakini ukarimu hauishii katika mwezi wa Ramadhani bali kwa mujibu wa ripoti za Maswahaba, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akizidisha ukarimu katika mwezi huu wa Ramadhani. Siku zote alikuwa mkarimu lakini alikuwa mkarimu zaidi katika mwezi huo.

Aidha ni muhimu kuzishirikisha pamoja familia zetu katika burudani za halali kama kusafiri pamoja kwenda kuona mbuga za wanyama sio tu kwa ajili ya kuosha macho na kufurahisha nafsi bali pia kupata ibra ya jinsi Allah alivyoumba maumbile ya wanyama mbalimbali, tembo aliowazidishia umbo, pundamilia aliowachora mistari, twiga aliyempa shingo ndefu na wengineo.

Katika kujenga na kuimarisha udugu wa Kiislamu, jambo jingine muhimu ni kushirikishana katika miradi ya Kiislamu. Tukishirikishana katika miradi hii kwa malengo ya kiharakati tutaimarisha udugu wetu.

Sumu mbaya sana ya kuuwa udugu wetu ni tabia ya utesi. Lazima tuepuke kabisa kusengenyana kwa sababu shetani hupanda kirahisi mbegu ya kuwafarakanisha Waislamu kupitia uovu huu wa utesi.

Utesi ni uovu mkubwa na adhabu yake ni kali. MwenyeiMungu anatuonya.
Wala baadhi yenu wasiwasengenye wengine. Je! Mmoja wenu anapenda kula nyama ya nduguye aliyekufa?” (49:12)

Tunaposengenya basi kwa vyovyote tunalengo la kumzungumza vibaya mtu fulani. Iwapo hatuna la maana la kusema basi ni bora tunyamaze kabisa. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema;
“yule aliyemuamini Allah na Siku ya Mwisho basi aseme mazuri au abaki kimya, na yule aliyemuamini Allah na siku ya Mwisho awe mkarimu kwa jirani yake. (Muslim).

Sote sisi tuwakosefu. Unaweza kufanya vizuri katika jambo moja na ukakosea katika jambo jingine. Hebu tusitiriane upungufu wetu. Ukifahamu kosa la nduguyo, usilisambaze na kulikuza.

Kama ni nduguyo wa dhati kwa nini usimuwaidhi kwa stara, hekima na mawaidha mazuri. Mkumbushe nduguyo kwa upole na mueleze namna wewe unavyoona uchungu yeye kuwa na upungufu huo. Mueleze kwa kutumia Hadith ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa wewe na yeye ni kiwiliwili kimoja hivyo anapoumia yeye na wewe pia unaumia.

Kwa kufanya hivyo sio tu utaepuka utesi bali MwenyeziMungu atakupa malipo bora kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:
yule anayehifadhi kasoro za mwingine katika dunia hii, naye kasoro zake zitahifadhiwa na Allah Siku ya Hukumu.” (imeafikiwa na wote).

Katika kujenga na kuimarisha udugu wa Kiislamu, ni muhimu pia kuepuka husuda na dhana mbaya. Kamwe tusioneane husuda. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:
“msikate ujamaa, msigeuke, msichukiane, na msihusudiane. Ninyi mkiwa ni  waja wa Mwenyezi Mungu, dumisheni udugu. Waislamu wawili wasinuniane kwa zaidi ya siku tatu” (Malik)

Pia si jambo zuri kujengeana dhana kwani MwenyeziMungu anasema:
“Enyi mlioamini Jiepusheni na dhana kwani dhana ni dhambi. (49:12)

Jingine ambalo ni muhimu katika kujenga na kudumisha udugu wa iman ni uungwana na unyenyekevu. Mara zote kuwa wa mwanzo kuomba radhi inapotokea hali ya kutokuelewana.

Hii itapunguza moto wa ugomvi na hatimaye kuuzima kabisa bila kuhitaji mtu mwingine wa kusuluhisha. Ndugu wawili wanapoudhiana na kukorofishana halafu wakatanabahi kuwa wao ni ndugu wanaopaswa kupendana na si kugombana, basi kila mmoja wao ajirejeshe kwa kuwahi kuomba radhi kabla ya mwenziwe. Kila mmoja aukimbilie haraka msamaha kabla ya mwenziwe ili mwenziwe asije kuonekana muungwana zaidi kuliko yeye.

Huu ni wema miongoni mwa mema tunayopaswa kushindana kwayo. Na huu ndio ufumbuzi halisi na wa kudumu wa migogoro. Vile vile kabla ugomvi haujazuka, ni muhimu kila mmoja kuwahi kuuepuka kabla ya mwenziwe, watajikuta wote wawili wakiepuka shari ya shetani kirahisi kabisa.

Ugomvi na ndugu yako si jambo la kulipania au kuliendea kifua mbele. Bali ugomvi na ndugu yako uwe pigo la kujutia moyoni. Ulete aibu usoni. Ugomvi uwazidishie haya na heshima  ndugu wawili wa imani. Siku zote kila mmoja ajihoji kwa nini kagombana na nduguye wa Kiislamu?

Hebu ndugu wawili wa imani, kabla ya kujibizana vibaya, kusemeshana ovyo au kukunjiana ngumi au hata kupigana, watazamane nyuso zao kisha nyoyo zao zijiulize haraka sana, je huyu ninayetaka kugombana naye si ndugu yangu ambaye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema, ni Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallama na kiwiliwili kimoja.

Kwa mantiki hiyo, je nikimtukana si nimejitukana mwenyewe! Nikimpiga kofi au ngumi si nimejipiga mwenyewe!Nikimuumiza si nimejiumiza mwenyewe! Nikimuumbua si nimejiumbua mwenyewe!

Nyoyo zikishatanabahi, kila mmoja, kwa masikitiko na bashasha ya huzuni, anyooshe mikono ya kukumbatiana na nduguye na akumbatiane naye. Huu ndio udugu wa Kiislamu. Hii ndiyo mantiki ya Mwenyezi Mungu kusema ameziunganisha nyoyo za Waislamu.

Zaidi ya hivyo mtu anayewahi kuomba msamaha ndiye anayelipwa na Allah. Kwa hiyo kuna faida nyingi katika jambo hili. Udugu wa nyoyo uwalize kilio cha machozi kwa nini wamegombana ilihali wao ni ndugu wa kuoneana uchungu, kujuliana hali, kusaidiana na kuzikana na ni ndugu ambao, InshaAllah, watakutana na kuishi pamoja maisha ya milele Peponi.

Katika kuimarisha udugu wa Kiislamu, ndugu wa Kiislamu wasipuuzie kutazamana kwa nyuso za bashasha na kusemeshana kwa upole. Kukunjiana nyuso si jambo jema na ni ishara ya uaduwi au chuki moyoni.

Wakati uso wa bashasha au uso wa furaha ya kukutana na nduguyo Muislamu hudhihirisha athari za mapenzi moyoni,  uso wa makunyanzi hujenga shaka ndani ya moyo wa nduguyo.

Pengine hataweza kukuuliza kwa nini umemkunjia uso au kwa nini umemnunia lakini moyoni atabaki na maswali mengi kwa nini ndugu yangu hakuonesha uso wa furaha nilipokutana naye? Nimemkosea nini? Au anachukizwa na nini katika wasifu na tabia yangu? Au hapendezwi na haiba yangu?

Kwa ujumla kutooneshana nyuso za bashasha kwaweza kusababisha dhana na hatimaye ndugu wawili kukosa mapenzi ya dhati baina yao huku kila mmoja akiwa hajui undani wa mwenziwe.

Mara zote ndugu wawili wasemeshane kwa maneno mema, maneno ya kiungwana, maneno ya kujenga udugu, maneno ya kuimarisha udugu. Katu wasikebehiane kwa chochote kile.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliikataa kauli ya Swahaba Mwarabu ya kumkebehi Swahaba mweusi. Alimdhihaki mwenziwe kwa sababu eti yeye ni mwarabu au tuseme mtu mweupe na mwenziwe ni mtu mweusi.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alipewa jukumu la kuwaunganisha wanadamu wote kwa kamba ya Uislamu, hakufurahishwa na kebehi hiyo. Na badala yake alifurahia jibu la yule aliyekebehiwa.

Swahaba mweupe alipojuta kwa kauli yake hiyo na kumtaka nduguye mweusi amlipizie kwa kumkanyagakanyaga kichwani, mwenziwe alikataa kwa kusema,asingeweza kukanyaga kichwa ambacho ndani yake kina Kalima “Laaila-ha illa-llah”.

Kwa maana nyingine Sahaba huyu alikuwa na maana kuwa yeye asingeweza kumkanyaga nduguye ambaye ndani ya moyo wake mna imani juu ya Allah na ambao umemkubali Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama Mtume Wake.

Alihisi kuwa kama angekinyaga kiwiliwili cha nduguye basi ingekuwa kama vile amekikanyaga kiwiliwili chake mwenyewe kwa kuzingatia ile Hadith ya Mtume kuwa waumini ni kama mwili mmoja, kiungo kimoja kikiumia basi mwili mzima huhisi maumivu.

Mtu aliyeshiba imani na aliyemshiba nduguye wa imani angewezaje kuona raha kumkanyaga nduguye huyo. Kwa hiyo nukta yetu ni kuwa kauli ya kebehi iliyotolewa na Sahaba mweupe ilihatarisha udugu na kauli ya Swahaba mweusi ikauweka salama udugu huo.

Kwa hiyo sote tuchunge sana kauli zetu. Haifai kabisa kukebehiana. Kama wewe ni  Mwarabu, mwafrika, mchina, Mzungu, Mjapan, Muhindi, hiyo ni sifa tu ya kukutambulisha kwa wengine lakini katika mizani ya imani, sifa hii haiongezi hata robo kilo ya amali za mtu.

Daraja la ubora wa mtu mbele ya yule aliyetuumba sisi sote halipatikani kwa uarabu wa mtu, uafrika wa mtu na kadhalika. Bali daraja linapatikana kwa mizani ya uchaMungu.

Ndio maana tunaonywa kuwa waumini wanaume kwa wanawake wasidharauliane kwa vigezo vya mali, kipato, rangi, kabila wala Taifa. Pengine yule anayedharauliwa ndiye mwenye daraja kubwa mbele ya MwenyeziMungu. Na wale wanaodharau wenzao kwa kigezo chochote miongoni mwa hivyo, ndiyo wenye daraja duni au pengine hawana daraja lolote.

Haya yakizingatiwa, kwa kweli, udugu wa kweli na wa dhati kabisa utajengeka miongoni mwa Wailamu wa leo kama ulivyojengeka miongoni mwa Waislamu waliopita.

Ndugu wa Kiislamu furahianeni na salimianeni kwa salamu ya amani, “Asalaam alaikum”. Wakati mkisalimiana nyuso zioneshane bashasha na ikiwezekana peaneni mikono au hata kukumbatiana.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema
tabasamu unayoonesha kwa nduguyo ni sadaka” (Tirmith).

Kwa kuhitimisha ifahamike kuwa mambo yote yanayohitajika katika kujenga na kuimarisha udugu wa Kiislamu yamo katika mafundisho ya Uislamu.

Kwa hiyo ni juu yetu kuyatia vitendoni, tukianza na nafsi zetu wenyewe. Kanuni nyepesi ya mahusiano yetu ya kindugu ni hii. “kadri tunavyozidi kuitekeleza dini yetu ndvyo tunavyokuwa na mazingira bora zaidi ya udugu wetu.
                MWENYEZI MUNGU ANAJUA ZAIDI

Sourec:Posted by Mwashabani Mrope via facebook.com on TANZANIA MUSLIM Grou

Comments :

0 comments to “YEPI YA KUIMARISHA UDUGU WETU WA KIISLAMU ?”

Post a Comment

 

Website Hit