Islamic Calender

Powered by Blogger.

HOJA YA TANO YA WATETEZI WA MAULID- Sehemu ya Pili


Sehemu ya Pili
HOJA YA TANO YA WATETEZI WA MAULID
Kwamba Maswahaba walimpokea Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipoingia Madiynah kwa qaswiydah na wengine walikuwa wakimsomea mashairi na qaswiydah Mtume صلى الله عليه وآله وسلم za kumsifu na yeye alikuwa akikubali kusomewa hayo mashairi.
Jibu la kwanza la Hoja hiyo:
Kwanza kuna shaka na usemi huo wa kusomewa qaswiydah ya 'Twala'al-Badru 'Alayna, Min Thaniyaatil Wada'a' wakati wa kupokelewa alipofika Madiynah. Historia za kuaminika za tukio hilo zinaonyesha hakuna ushahidi kuwa Mtume alipita njia hiyo ya 'Thaniyat al Wada'a' wakati wa kuelekea Madiynah, na hali qaswiydah hiyo inaelezea mapitio yake ya sehemu hiyo!
Jibu la pili la Hoja hiyo:
Haikuthibitika kwamba Maswahaba walikuwa wakimsomea mashairi na qaswyidah siku ya kuzaliwa kwake, bali ilikuwa zaidi kunapotokea ushindi wa vita kuwashinda maadui.

HOJA YA SITA YA WATETEZI WA MAWLID
Kwamba kusherehekea Mawlid ni kumpenda, kumuadhimisha, kumtukuza na ni kumbukumbu ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kwa watu, na hili ni jambo linalotupasa tufanye ili vizazi vyetu pia vipate kumtambua Mtume صلى الله عليه وآله وسلم:
Jibu la kwanza la Hoja hiyo:
Kumkumbuka na kumuadhimisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kunatupasa kila siku katika maisha yetu kwa kumpenda na kufuata Sunnah zake. Na si kwa njia ya kusherehekea kama inavyosherehekewa kwa kusoma Mawlid mara moja tu katika mwaka.
Jibu la pili la Hoja hiyo:
Kumbukumbu ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kwa watu na vizazi vyetu vimeshabainishiwa na Allaah سبحانه وتعالى katika Qur-aan na Sunnah. Nayo ni kwa kila siku vile vile na si kwa mwaka mara moja tu. Katika Qur-aan Anasema Allaah سبحانه وتعالى
((وَرَفَعْنَا لَكَ ذِكْرَكَ))
((Na Tukakutukuza utajo wako)) [Ash-Sharh:4]
Na kutukuzwa huko ni katika kila Swalah zetu tunapomswalia katika tashahhud, katika kutimiza fardhi zetu kama Hajj na Swawm, inapoadhiniwa na iqaamah ya Swalah, kwenye khutba, kumswalia anapotajwa jina lake, tunaposoma au kusikia Hadiyth zake, katika kufuata Sunnah zake, katika vikao vya darsa za dini yetu na kadhalika, kwa hiyo ni kumbukumbu ya kila siku, kila wakati katika maisha yetu na sio siku moja tu katika mwaka.


HOJA YA SABA YA WATETEZI WA MAULID
Kwamba kuna Bid'atun-hasanah (bid'ah njema).
Jibu la hoja hiyo:
Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipotaja kuhusu bid'ah amesema:
((....وإِيَّاكُمْ ومُحْدثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٍ ضلالَةٌ )) رواه أبو داود ، والترمذِي وقال حديث حسن صحيح
((…na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu)) [Abu Daawuud, At-Trimidhiy kasema Hadiyth hasan sahiyh]
Hapa ametaja kuwa 'Kullu bid'atin Dhwalaalah' (KILA bid'ah ni upotofu). Na ikiwa kauli hii wanaipinga kuwa si KILA bid'ah, basi wanasemaje kuhusu kauli za Allaah سبحانه وتعالىAnaposema:
((كُلُّ نَفْسٍ ذَآئِقَةُ الْمَوْتِ))
((Kila nafsi itaonja mauti)) [Al-'Imraan: 185]
((وَكُلَّ إِنسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَآئِرَهُ فِي عُنُقِهِ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا ))
((Na kila mtu Tumemfungia amali yake shingoni mwake. Na Siku ya Qiyaamah Tutamtolea kitabu atakachokikuta kiwazi kimekunjuliwa)) [Al-Israa:13]
((كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ))
((Kila nafsi imo rahanini kwa mabaya iliyoyachuma)) [Al-Mudathhir:38]
((وَكُلُّ شَيْءٍ فَعَلُوهُ فِي الزُّبُرِ)) ((وَكُلُّ صَغِيرٍ وَكَبِيرٍ مُسْتَطَرٌ))
((Na kila jambo walilolifanya limo vitabuni))
((Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa)) [Al-Qamar:52-53]
Je, tutakanusha kwamba sio kila nafsi itaonja mauti, au si kila mtu amefungiwa amali zake shingoni, au si kila nafsi iko rahanini, au si kila jambo tunalolifanya dogo na kubwa liko vitabuni? Bila shaka kauli ya Allaah سبحانه وتعالى Inathibitisha kuwa kila binaadamu atakufa na kila mmoja ana hesabu yake atakayoikuta siku ya Qiyaamah. Kwa hiyo na kauli ya 'kullu bid'atin dhwalaalah' (kila bid'ah ni upotofu) pia ina maana kwamba hiyo hiyo bila ya kuigawa ikawa ni baadhi tu ya bid'ah.

HOJA NA NANE YA WATETEZI WA MAWLID
Kwamba kuna baadhi ya mambo yamefanyika baada ya kufa kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na yanaendelea kutendeka kwa hiyo ni bid'ah. Mifano wa hayo yanayotolewa kama hoja ni; kukusanywa Qur-aan na kuwekwa katika mus-haf na Abu Bakar رضي الله عنه kuhamishwa Maqaam Ibrahiym na 'Umar ibnul Khatwaab رضي الله عنه au kuongezwa adhaan ya pili na ya tatu siku ya Ijumaa na 'Uthmaan bin 'Affaan رضي الله عنه
Jibu la Hoja hiyo:
Kwamba jambo lolote walilolifanya hao Makhalifa ni Sunnah za kuzifuata pia kama Alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :
((... أُوصِيكُمْ بِتَقْوى اللَّه، وَالسَّمْعِ وَالطَّاعَةِ وإِنْ تَأَمَّر عَلَيْكُمْ عَبْدٌ حبشيٌ، وَأَنَّهُ مَنْ يَعِشْ مِنْكُمْ فَسَيرى اخْتِلافاً كثِيرا . فَعَلَيْكُمْ بسُنَّتي وَسُنَّةِ الْخُلُفَاءِ الرَّاشِدِينَ الْمَهْدِيِّينَ ، عضُّوا عَلَيْهَا بالنَّواجِذِ، وإِيَّاكُمْ ومُحْدثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٍ ضلالَةٌ) رواه أبو داود ، والترمذِي وقال حديث حسن صحيح
((Nakuusieni kumcha Allah, usikivu na twaa hata ikiwa kiongozi wenu (Au atakayekuamrisheni) ni Mtumwa wa Kihabashi. Mtakaoishi miongoni mwenu mtaona ikhtilafu nyingi. Kwa hiyo shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waliongoka baada yangu. Ziumeni kwa magego (zikamateni kwa nguvu wala msiziache). Na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu) [Abu Daawuud, At-Trimidhiy kasema Hadiyth hasan sahiyh]

HOJA YA TISA YA WATETEZI WA MAWLID
Kwamba msahafu ulikuwa hauna irabu/harakaat (vokali), au Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na Maswahaba hawakutumia kipaza sauti (speakers) katika adhaan, au kufanya twawaaf juu badala ya chini, au hawakupanda magari bali walipanda ngamia, au hakukuweko na zana za utamaduni za kujifunza dini kama radio, televisheni, mtandao, tovuti, CD's na kadhalika. Kwa hiyo kutumia vitu hivyo pia ni bid'ah.


Jibu la Hoja hiyo:
Kuhusu Mus-haf na irabu – Qur-aan ilikuwa imehifadhiwa katika vifua vya Maswahaba ambao walikuwa ni wenye lugha ya Kiarabu fasaha, kwa hiyo hawakuhitaji irabu. Ilipotokea haja ya kukusanya Qur-aan katika mus-haf kwa vile Maswahaba wengi waliohifadhi Qur-aan waliuliwa katika vita vya Yamaamah, Maswahaba wakaingiwa na khofu ya kupotea Qur-aan kabisa hata isiweze kutufikia sisi na vizazi vyote hadi siku ya Qiyaamah. Ndipo ilipokusanywa baada ya ushauri mzito baina ya Makhalifa na Maswahaba na wakakubaliana kuikusanya katika Mus-haf.
Hata hivyo kukawa vile vile hakuna haja ya kuweka irabu kutokana na ufasaha wa lugha ya Kiarabu. Ilipofikia zama za Yusuf bin Hajjaaj, khofu iliingia ya kutowezekana kuisoma Qur-aan inavyopasa kwa vile lugha ya Kiarabu ilianza kupotea ufasaha wake. Kwa hiyo jambo kama hili lilikuwa ni jambo lililohitajika kufanyika ili kuendeleza ibada ya kuisoma Qur-aan na kupata mafunzo yake, na khaswa kwamba Qur-aan ni uongofu wa ulimwengu mzima, hivyo hata ambao si Waarabu waweze kuisoma baada ya kuweka irabu/harakaat, la sivyo ingelikuwa vigumu kusomeka kwa wasiojua lugha ya Kiarabu sawa sawa.
Hali kadhalika kufanya twawaaf juu kumehitajika na kumekuwa hakuna budi, kwa umuhimu wa kutimiza ibada hiyo ya fardhi, na kutokana na zahma kubwa ya Mahujaji haiwezekani wote kutimiza twawaaf chini. Kwa hiyo panapotokea umuhimu wa jambo la lazima kufanyika kwa manufaa ya Ummah wa Kiislamu ili tuweze kutimiza ibada zetu basi hakuna budi kutendeka na hata hivyo haiingii katika kuzidisha ibada yenyewe khaswa.
Ama kuhusu nyenzo kama vipaza sauti, njia za usafirishaji, vifaa vya utamaduni vya kujifunzia na kadhalika vyote hivyo ni nyenzo tu za kutuwepesishia kutekeleza ibada zetu na yote yanayotupasa katika amri za dini. Kuchanganya nyenzo na ibada ni jambo lilisilokuwa la mantiki (logic). Na Allaah سبحانه وتعالى Mjuzi wa mambo yasiyoonekana Amejua yote hayo kuwa yatatokea. Mfano kuhusu usafiri Allaah سبحانه وتعالى Amejua kwamba watu watatoka kila pembe ya dunia kufika Makkah kutimiza Hajj, sasa vipi mtu ategemee kuwa usafiri wa nchi ya kutoka Kaskazini kufika Kusini asafiri na mnyama? Bila shaka haingii akilini jambo hili.
Hivyo Allaah سبحانه وتعالى Ametambua shida ya usafiri zitakazotokea kutokana na umbali wa nchi na nchi ndio Akasema:
((وَالأَنْعَامَ خَلَقَهَا لَكُمْ فِيهَا دِفْءٌ وَمَنَافِعُ وَمِنْهَا تَأْكُلُون))
((وَلَكُمْ فِيهَا جَمَالٌ حِينَ تُرِيحُونَ وَحِينَ تَسْرَحُونَ))
((وَتَحْمِلُ أَثْقَالَكُمْ إِلَى بَلَدٍ لَّمْ تَكُونُواْ بَالِغِيهِ إِلاَّ بِشِقِّ الأَنفُسِ إِنَّ رَبَّكُمْ لَرَؤُوفٌ رَّحِيمٌ))
((وَالْخَيْلَ وَالْبِغَالَ وَالْحَمِيرَ لِتَرْكَبُوهَا وَزِينَةً وَيَخْلُقُ مَا لاَ تَعْلَمُونَ))
((Na wanyama hao Amekuumbieni. Katika hao mna vifaa vya kutia joto, na manufaa mengineyo, na baadhi yao mnawala))
((Na wanakupeni furaha pale mnapowarudisha jioni na mnapowapeleka malishoni asubuhi))
((Na hubeba mizigo yenu kupeleka kwenye miji msiyoweza kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi. Hakika Mola wenu Mlezi ni Mpole na Mwenye kurehemu))
((Na farasi, na nyumbu, na punda ili muwapande, na kuwa ni pambo. Na Ataumba msivyovijua)) [An-Nahl:5-8]
Tusivyovijua ndio kama njia za usafiri za kisasa kama magari, ndege, matreni na kadhalika [Aysarut-Tafaasiyr Shaykh Abu Bakr Al-Jazaairy: 3:102]
Kwa hiyo kila inapopatikana njia au kifaa bora cha kutusahilishia maisha yetu kinafaa kutumika na haiwi ni jambo la bid'ah katika dini, bali unaweza kuita bid'ah kilugha kwani hivyo sio ibada iliyokusudiwa kuwa ni bid'ah.
Tukimalizia, tunaona kwamba hoja zote hizo zitolewazwo na wanaounga mkono Mawlid si sahihi, bali ni za kujaribu kulipa jambo hilo sheria na hali halimo katika sheria katu. Na wengi wengine watakwambia, "Kwani kuna ubaya gani?" Au watakutuhumu wewe unayewauliza ushahidi wa kufanya jambo hilo, kuwa humpendi Mtume صلى الله عليه وآله وسلم.
Lau kama kusherehekea mazazi yake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ingelikuwa ni amali njema, basi Maswahaba na Salaf Swaalih (wema waliopita) wangelitutangulia katika jambo hilo. Wao walikuwa wakizielewa mno Sunnah za Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuliko sisi, walimpenda mno kuliko sisi, na walikuwa tayari kupoteza nafsi zao au mali zao kwa mapenzi yao kwake, na walifuata sheria kuwashinda wale waliokuja baada yao.

Sisi tumeamrishwa 'kufuata' na tumekatazwa 'kuzua'. Hii ni kwa sababu ukamilifu wa dini ya Kiislamu na utoshelezaji wa yale tuliyopewa na Allaah سبحانه وتعالى na Mtume Wake, na hayo yamefuatwa na Waislam wote wa mwanzo kuanzia Maswahaba na wafuasi wao wema.
اللَّهُمَّ اَرِنا الْحَقَّ حَقاً وَارْزُقْنا اتِباعَه وَارِنا الباطِلَ باطلاً وَارْزُقْنا اجْتِنابه .
Allaahumma Arinal-Haqqa Haqqaw-War-Zuqnat-tibaa'ah, Wa Arinal-Baatwila Baatwilaw-War-Zuqnaj-tinaabah.
Ee Allaah, Tuonyeshe haki kuwa ni haki Na Uturuzuku kuifuata. Na utuonyeshe batili kuwa ni batili na Uturuzuku kuiepuka

Comments :

0 comments to “HOJA YA TANO YA WATETEZI WA MAULID- Sehemu ya Pili”

Post a Comment

 

Website Hit