Islamic Calender

Powered by Blogger.

Nguzo tano za uislam

Nguzo tano za uislam
1) Shahada ya Imani
Ushahidi wa Imani ni kusema kwa kusadikisha, La ilaaha illAllaah, Muhammadur Rasulullah.” Maana ya matamshi haya ni, “Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu (Allaah), na kwamba Muhammad ni Mjumbe (Mtume) wa Mwenyezi Mungu.” Sehemu ya kwanza, “Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki, isipokuwa Mwenyezi Mungu,” inamaanisha kwamba hapana mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu peke Yake, na kwamba Yeye hana mshirika wala mwana. Ushahidi huu wa Imani unaitwa Shahada, ambayo ni kanuni nyepesi ambayo inapaswa itamkwe pamoja na kusadiki ili mtu aweze kuingia katika Uislamu, kama ilivyoelezwa hapo juu. Ushahidi wa Imani ndio nguzo muhimu zaidi katika Uislamu.
2) Swalah
Waislamu huswali Swalah tano kila siku. Kila Swalah huchukuwa muda mfupi wa dakika chache tu. Swalah katika Uislamu ni mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mja na Mwenyezi Mungu. Hakuna kishenga baina ya Mwenyezi Mungu na mfanyaji ibada.
Ndani ya Swalah, mtu hujisikia ndani mwake furaha, amani na faraja, na kwamba Allaah yu radhi naye. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Bilaal adhini, ili tufarijike nayo.))[109] Bilaal alikuwa mmojawapo wa Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na alikuwa mwadhini.
Swalah hufanyika wakati wa Alfajiri, Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na ‘Ishaa. Muislam anaweza kuswali karibu mahali popote, kama vile mashambani, ofisini, viwandani au vyuoni.
Tafadhali, tembelea kwa ajili ya maelezo zaidi juu ya Swala katika Uislamu
3) Kutoa Zakaah (Kuwakunjulia Wenye Dhiki):
Kila kitu ni cha Mwenyezi Mungu, na hata mali zinazohifadhiwa na wanaadamu kama dhamana. Maana khalisi ya neno Zakaah ni zote mbili ‘kutwaharisha’ na ‘kukua.’ Maana ya kutoa Zakaah ni kutoa asilimia iliyotajwa bayana kutokana na mali fulani kwa kuwapatia makundi fulani ya watu wenye dhiki. Asilimia inayopaswa kulipwa kutokana na dhahabu, fedha na pesa taslimu zenye kufikia kiasi kinacholingana na gramu 85 za dhahabu na kubaki katika miliki ya mtu kwa mwaka mmoja wa Kiislamu ni asilimia mbili unusu. Tunavyovimiliki hutakasika kwa kutenga pembeni sehemu ndogo tu kwa ajili ya wenyedhiki, na kama vile kupogoa matawi ya mimea, huku kupunguza salio na kunatia moyo wa ukuaji mpya.
Mtu anaweza kutoa zaidi kadiri atakavyo kama Sadaka.
4) Kufunga katika Mwezi wa Ramadhaan Kila mwaka katika mwezi wa Ramadhaan,Waislamu hufunga tangu Alfajiri hadi kuchwa kwa jua, kwa kujizuia kula, kunywa na tendo la ndoa.
Ingawa Swawm ni yenye faida za kiafya, huchukuliwa kimsingi kuwa ni namna ya kuisafisha nafsi kiroho. Kwa mmojawapo kujizuia dhidi ya starehe za kidunia, japo kwa muda mfupi, mfungaji hupata huruma ya kweli kwa wanaopatwa na njaa, kadhalika na kuongezeka kwa maisha yake ya kiroho.
5) Kuhiji Makkah:
Hija ya kila mwaka Makkah ni faradhi ya kufanywa mara moja tu maishani kwa wenye uwezo wa kimwili na mali katika kuitekeleza. Kadiri ya watu milioni mbili huenda Makkah kila mwaka kutoka kila sehemu duniani. Ingawa mara zote Makkah huwa imesheheni wageni, Hija ya mwaka hufanywa katika mwezi wa kumi na mbili katika kalenda ya kiislamu. Mahaji wa kiume huvaa nguo maalumu na rahisi ambayo huondosha mbali tofauti za kimatabaka na tamaduni kiasi kwamba wote huwa sawa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Source:Al-Hidaya

Comments :

0 comments to “Nguzo tano za uislam”

Post a Comment

 

Website Hit