Islamic Calender

Powered by Blogger.

HOJA ZA WANAOSHEREHEKEA MAWLID-Sehemu ya Kwanza


Sehemu ya Kwanza
HOJA ZA WANAOSHEREHEKEA MAWLID NA MAJIBU YAKE
HOJA ZA WANAOSHEREHEKEA MAWLID NA MAJIBU YAKE

Ummu Iyyaad
BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa ba’ad:
Tunaandika makala hii kwa ikhlaasw na unyenyekevu kabisa mbele ya Allaah سبحانه وتعالى kisha mbele ya ndugu zetu wanaodhani kwamba kushereheka Mawlid ni jambo jema na si jambo la bid'ah.
Niya yetu ni kutaka kuwatanabahisha ndugu zetu Waislamu kuhusu mas-ala yaliyoingia shubuhaat na yanayoharibu 'Aqiydah ya Muislamu kwani kama wanavyosema Maulamaa kuwa ufisadi mkubwa wa dini ni uzushi (bid'ah) wa mambo katika dini. Kwa hiyo tunataka kuwaonyesha ndugu zetu yaliyo baatil na ya haki ili wabakie katika 'Aqiydah safi na mwendo wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na Maswahaba zake.
Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba mas-ala haya ya kuonyesha yaliyo sahihi na kukataza bid'ah yanaleta kufarikiana Ummah huu, hata kufikia kuzozana baina ya Waislamu. Tunachopenda kuwakumbusha ndugu zetu ni kwamba huu ni ujumbe tunaofikisha na hali tukiamini ni wa haki ingawa unakubali kukosolewa, na ni juu ya msomaji mwenyewe kuamua kuufuata au kuuacha lakini bila ya kufarikiana, bali ubakie undugu na ihsaan baina yetu bila ya kuingia chuki au kutengana.
Tufahamu kuwa Allaah سبحانه وتعالىAmetuamrisha jambo la kuamrishana mema na kukatazana mabaya na ndio iwe kazi yetu kama Anavyosema:
((وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ))
((Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu)) [At-Tawbah:71]
Na vile vile ni kutimiza amri ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliyotuambia kwamba:

عن أَبي سعيدٍ الخُدْريِّ رضي اللَّه عنه قال : سمِعْتُ رسُولَ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم يقُولُ : ((مَنْ رَأَى مِنْكُم مُنْكراً فَلْيغيِّرْهُ بِيَدهِ ، فَإِنْ لَمْ يَسْتَطعْ فبِلِسَانِهِ ، فَإِنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَبقَلبهِ وَذَلَكَ أَضْعَفُ الإِيمانِ)) رواه مسلم .

Kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudhriy رضي الله عنه
ambaye amesema: Nilimsikia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akisema: ((Yeyote yule atakayeona kitendo kiovu mwache akiondoe (abadilishe) kwa mkono wake, ikiwa hawezi basi kwa ulimi wake (alikemee au kukataza), na ikiwa hawezi basi kwa moyo wake (achukie) na huo (yaani kuona baya na kunyamaza) ni udhaifu wa Imani)) [Imesimuliwa na Muslim]
Hatuna budi kufuata uongozi katika ibada kwa njia aliyotufundisha Mtume

صلى الله عليه وآله وسلم kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى:
((لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ))

((Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho)) [Al-Ahzaab:21]

Na Anasema Allaah سبحانه وتعالى

((وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا))

((Na anachokupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho)) [Al-Hashr: 7]
Naye Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametuamrisha katika nasw nyingi tumfuate katika ibaada, mbili zifuatazo:

((صلوا كما رأيتموني أصلي))

((Swalini kama mlivyoniona naswali)) [Al-Bukhaariy]

((يا أيها الناس خذوا عني مناسككم)) صحيح الجامع

((Enyi watu, chukueni kwangu manaasik zenu [utaratibu wa ibada ya Hajj])) [Muslim]
Na Ametuonya kwamba tukifanya kitendo kilichokuwa si katika mwendo wake na Maswahaba zake basi hakina thamani, bali hakitapokelewa:
(( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري
((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa)) [Muslim]

HOJA YA KWANZA YA WATETEZI WA MAWLID
Aayah katika Surat Yuunus:

((قُلْ بِفَضْلِ اللّهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَلِكَ فَلْيَفْرَحُواْ هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ))

((Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na Rehma yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya)) [Yuunus:58]
Jibu la kwanza la Hoja hiyo:
Baadhi ya watetezi wa Mawlid wanatoa hoja ya Aayah hii kuwa kuambiwa na Allaah سبحانه وتعالىwafurahi, basi ni kufurahia mazazi ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم. Lakini tukitazama tafsiri ya Aayah hiyo kwa wafasiri wote wakubwa kama Ibnu Jariyr, Ibnu Kathiyr, Qurtubiy, Al-Baghaawiy, Ibnul-Arabiy na wengineo, hatukuti maana hiyo kabisa. Maana iliyotajwa na wafasiri ni wafurahi kwa yale yaliyowajia kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى ya uongofu na dini ya haki. Na pia imefasiriwa kuwa, wafurahi kwa Qur-aan na Uislam. Ushahidi ni kutokana na Aayah ya kabla yake inayosema:

((يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاء لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ))

((Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uongofu, na Rehma kwa Waumini)) [Yuunus:57]
Nayo ni Qur-aan. Na kama pia Aayah ya 170 ya Suratul 'Imraan isemayo, ((Na ni wenye kufurahia fadhila Zake)). Vilevile imefasiriwa kuwa fadhila Zake ni Uislam, na Rahma Zake ni Qur-aan. wa Allaahu A'alam
Amesema Ibnu Kathiyr katika tafsiyr yake kuhusu: ((uongofu na Rahma kwa Waumini)), ni kupata uongofu na Rahma kwa waumini waliosadiki na kukinaika. Kama zinavyoonyesha kauli Zake Allaah سبحانه وتعالى nyingine:

((وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِلْمُؤْمِنِينَ وَلا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَاراً))

((Na Tunateremsha katika Qur-aan yaliyo ni matibabu na Rehma kwa Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara)) [Al-Israa:82]
Na kauli Yake Allaah :سبحانه وتعالى
((قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدىً وَشِفَاء))
((Sema: Hii Qur-aan ni uongofu na poza kwa wenye kuamini)) [Fuswilat:44]
Jibu la pili la Hoja hiyo:
Rahma kwa watu haiwi kwa mazazi ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم bali ni kwa kupewa kwake Utume na kutumwa kufikisha ujumbe kwa watu. Na dalili ni kutoka katika Qur-aan na Sunnah.
Nasw kutoka katika Qur-aan ni kwamba yeye ni Rahma kwa viumbe wote kutokana na kutumwa kwake na wala haikutaja kuzaliwa kwake. Anasema Allaah سبحانه وتعالى
((وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ))
((Nasi Hatukukutuma ila uwe ni Rehma kwa walimwengu wote)) [Al-Anibyaa:107]
Ama katika Sunnah ni Hadiyth:

عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: قيل : يا رسول الله ! ادع على المشركين . قال صلى الله عليه وسلم (( إني لم أبعث لعانا وإنما بعثت رحمة)) مسلم
Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه ambaye amesema: Aliambiwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم "Waombee (walaaniwe) Washirikina". Akasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ((Mimi sikupewa utume (sikutumwa kuja kuwa) ni mlaaniji (mwenye kuwaombea laana watu) bali nimepewa utume kuwa ni Rahma)) [Muslim]

HOJA YA PILI YA WATETEZI WA MAWLID
Aayah katika Suratul-Ahzaab
((إِنَّ اللَّهَ وَمَلائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيماً))
((Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamswalia Nabii. Enyi mlioamini! Mswalieni na mumsalimu kwa salamu)) [Al-Ahzaab:56]
Kwamba Mawlid yanahusu kumswalia kama ilivyo Aayah hiyo.
Jibu la kwanza la Hoja hiyo:
Imaam Al-Bukhaariy anatueleza tafsiri ya Aayah hiyo ni kuwa Maswahaba رضي الله عنهم walimuuliza Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuwa washajua namna ya kumtakia amani juu yake, lakini hawakujua namna gani wamswalie. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akawaambia waseme, 'Allahumma Swalli 'alaa Muhammad wa 'ala aali Muhammad...' hadi mwisho kama ilivyo kwenye tashahud.
Na maana au tafsiri ya Aayah hiyo imeelezwa na wafasiri na wana Hadiyth taqriban wote kwa maana hiyo au karibu na hiyo ya Imaam Al-Bukhaariy. Kwa maana hiyo tunakutana na ulinganisho usiolingana unaofanywa na watetezi wa jambo hilo.
Jibu la pili la Hoja hiyo:
Inatupasa tumsawalie Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kwa wingi kila mara kama ilivyothibiti fadhila zake katika Hadiyth ifuatayo:
عنْ عبد اللَّه بن عمرو بن العاص ، رضي اللَّه عنْهُمَا أنَّهُ سمِع رسُول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم يقُولُ : (( من صلَّى عليَّ صلاَةً ، صلَّى اللَّه علَيّهِ بِهَا عشْراً)) رواهُ مسلم
Imetoka kwa 'Abdullah ibn 'Amru ibn Al-'Aasw رضي اللَّه عنْهُمَاkwamba kamsikia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم anasema, ((Atakayeniswalia (kuniombea Rahma) mara moja, Allaah Atamswalia (Atampa Rahma) mara kumi)) [Muslim]
Kisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametufundishia nyakati za kumswalia kama siku ya Ijumaa, baada ya adhaan, anapotajwa n.k. Lakini hakutufundisha kuwa tumswalie siku ya kuzaliwa kwake.

HOJA YA TATU YA WATETEZI WA MAWLID
Kufurahikia kuzaliwa kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ni jambo lililoamrishwa katika Qur-aan wakitaja Aayah mbili zifuatazo zinazohusiana na Nabii Yahya عليه السلام na Nabii 'Iysa :عليه السلام
((وَسَلَامٌ عَلَيْهِ يَوْمَ وُلِدَ وَيَوْمَ يَمُوتُ وَيَوْمَ يُبْعَثُ حَيًّا))
((Na amani iwe juu yake siku ya kuzaliwa, na siku ya kufa, na siku ya kufufuliwa)) [Maryam: 15] Akimaanishwa Yahya عليه السلام
((وَالسَّلَامُ عَلَيَّ يَوْمَ وُلِدتُّ وَيَوْمَ أَمُوتُ وَيَوْمَ أُبْعَثُ حَيًّا))
((Na amani iko juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa, na siku nitakayofufuliwa kuwa hai)) [Maryam: 33] Akimaanishwa 'Iysa عليه السلام
Jibu la kwanza la Hoja hiyo:
Aayah inasema ((amani...)). Je, ina maana kwamba, neno 'amani' ni sawa na kufurahikia? Vile vile Aayah hizo hazikutaja kuzaliwa peke yake bali zimetaja; kuzaliwa, kufa na kufufuliwa. Sasa vipi ichukuliwe utajo mmoja tu na nyingine ziachwe? Vile vile Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amefariki mwezi huu wa Rabiy'ul Awwal na kama walivyokubaliana Maulamaa kwamba ni tarehe hiyo ambayo inayodaiwa kuwa kazaliwa, nayo ni 12 Rabiy'ul Awwal, ingawa uhakika wa kuzaliwa kwake haujulikani kama ni siku hiyo. Na je, wanaosherehekea kuzaliwa kwake vile vile wanasherehekea kufa kwake na kufufuliwa kwake? Ikiwa ni hivyo, vipi watasherehekea siku ya kufufuliwa kwake?

HOJA YA NNE YA WATETEZI WA MAULID:
Kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akifunga siku ya Jumatatu ambayo ilikuwa siku ya kuzaliwa kwake kama ilivyokuja nasw katika Hadiyth ifuatayo, kwa hiyo aliiadhimisha siku ya kuzaliwa kwake:
عن أبي قتادة رضي الله عنه : أن النبي صلى الله عليه وسلم سئل عن صوم يوم الاثنين فقال: ((ذلك يوم ولدت فيه وأنزل علي فيه)) رواه الإمام مسلم
Imetoka kwa Abu Qataadah رضي الله عنهkwamba aliulizwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuhusu kufunga Jumatatu akasema: ((Hiyo ni siku niliyozaliwa na siku ulioteremshwa kwangu [Utume])) [Imaam Muslim]
Kwa hiyo alikuwa akimshukuru Allaah سبحانه وتعالى kwa neema hiyo.
Jibu la kwanza la Hoja hiyo:
Kuiadhimisha siku yake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ya kuzaliwa na kumshukuru kulikuwa ni kwa kufanya ibada kama hiyo ya kufunga na sio kwa kusherehekea kusoma Mawlid.
Jibu la pili la Hoja hiyo:
Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hakufunga siku maalum katika mwezi huu wa Rabiy'ul Awwal ikiwa ni tarehe 12 au nyingine yoyote, bali alikuwa akifunga kila Jumatatu mwaka mzima.
Jibu la tatu la Hoja hiyo:
Kufunga kwake Jumatatu kwa ajili ya kumshukuru Allaah سبحانه وتعالى kupewa Utume awe 'mbashiriaji na muonyaji' kwa ulimwengu wote kulikuwa ni kwa kufunga pekee na si kwa kukusanya watu kwa kufunga au kusherehekea kama inavyosherehekewa na wasomaji Mawlid.

Comments :

0 comments to “HOJA ZA WANAOSHEREHEKEA MAWLID-Sehemu ya Kwanza”

Post a Comment

 

Website Hit